Mwanga, almaarufu 'Fumo', ni kijana mdogo ambaye hana hakika na asili wala
fasili yake. Yeye ni msi baba, msi mama. Anachokifahamu ni kwamba
'aliokotwa' kutoka katika makao ya mayatima. Licha ya kuwa yeye ni kiokote,
mlezi wake anampa kila kinachostahili kwa mtoto mwenye wazazi wote.
Hali inapoonekana kutakata, msiba baada ya msiba unabisha. Mlezi wake wa
pekee ambaye anamjua kama 'mama' anapigwa kalamu. Nyumba yao inauzwa
kwa wenye nacho. 'Dada yake' Fumo ananajisiwa na kubaki hali mahututi
katika mshikemshike wa kufurushwa kutoka kwa nyumba yao na wahuni
walioletwa na mmiliki mpya. Baadaye, mlezi wa Mwanga anafunguliwa
mashtaka ya kusingiziwa ili asiweze kufuata kesi ya kufutwa au kufurushwa
kutoka kwa nyumba yake. Mwanga na 'familia' yake wanajipata katika mitaa
ya vitongoji duni. Choo ni cha 'kurusha fataki' na bafu ni upenuni. Hamna stara
tena!
Akiwa shuleni, Mwanga anafanya bidii ya mchwa na kupita vyema, lakini
mikosi bado haimwachi akapumua. Huku akicheza na watoto wengine,
anajipata amekanyaga kilipuzi na kupoteza mguu wake. Lakini bidii yake na
kudura za Mwenyezi Mungu vinamwezesha kuwa mwanasheria nguli. Azma
yake sasa ni kutetea haki licha ya kilema chake. Kumbe kufa si kufariki, kufa
ni kuoza utumbo!
Hii ni riwaya ya kusisimua yenye kutia matumaini katika jamii iliyotamauka
kutokana na matatizo mengi yanayoletwa na ufisadi na kupotoka kwa
maadili.