King'ora cha Mwehu ni tamthilia inayoangazia matatizo ya
kiuchumi, kisiasa na kijamii yanayotokana na utawala mbaya wa
viongozi wa nchi ya Sifuri. Viongozi hawa hawana chochote wala
lolote la kuwafaidi wananchi au nchi zao. Kinachowaongoza ni
ulafi na kupapia kila kinachopatikana nchini na kudai wana haki
ya kusherehekea utamu wa Keki ya Taifa.Wanafanya hivi huku
wananchi wakiendelea kuumia, kuteseka na kudhalilishwa na
umaskini, njaa, ukosefu wa ajira miongoni mwa matatizo mengi
yaliyokuwapo tangu enzi za kupigania uhuru. Lakini wananchi
hawana njia ya kujinasua. Kila anayesema ng'we, anapata cha
mtema kuni.
Mwehu anapoliza king'ora chake, wengi wanampuuza na kudhani
ni mwehu tu, lakini hoja zake zinapelekea kuzinduka kwa umma.
Bi Kurwa na Mlevi wanajiunga na Mwehu, na hatimaye chachu ya
mabadiliko inakolea. Kumbe jamii inaweza kubadilishwa na
mwehu! Je, mwamko huu utazua kitu gani? Hii ni tamthilia ya
kimapinduzi. Ni kurunzi ya jamii.